Sunday, October 18, 2015

SELOUS AJALI YA HELIKOPTA WAKATI WAKAMPENI UCHAGUZI MKUU 2015.

HELIKOPTA ILIYO ANGUKA NAKUPELEKEA VIFO VYA: Aliyekuwa Mbunge wa jimbo la Ludewa, Mhe. Deo Filikunjombe (43), Plasdius Ngabuma Haule na Egdi Francis Mkwera aliyetajwa kuwa Ofisa Tawala wa Wilaya ya Tarime na rubani Kapteni William Silaa.



Chopa iliyo kuwa ikitumiwa na Mbunge wa CCM jimbo la Ludewa  Deo Filikunjombe ilianguka usiku tarehe 15/10/2015 na kulipuka kwenye mbuga ya Wanyama ya Selous.
Kwa mujibu wa Waziri wa maliasili na utalii Lazaro Nyalandu alithibitisha kwamba mmoja wa waliokuwemo ndani ni Mbunge wa Ludewa Deo Filikunjombe.

Mh. Deo Filikunjombe
1972 - 2015
Waziri Nyalandu


Kupitia  ukurasa  wake  wa  Twitter,Nyalandu  aliandika;
“Tumetuma vikosi vya maafisa na maaskari katika eneo la Selous kulikotokea ajali ya helikopta katika harakati za uokozi, ajali ya helikopta imetokea katika kitalu R3 ndani ya mbuga ya Selous na mashuhuda wanasema ilianguka na kulipuka ng’ambo ya mto Ruaha....

 Mashuhuda wa ajali ya helikopta iliyotokea Selous walikuwa kitalu R2 na walishuhudia ikianguka na kulipuka ng’ambo ya mto Ruaha Kitalu R3, Maafisa na Maaskari wanaelekea eneo la tukio kutokea Msolwa na Matambwe na tumeagiza vikosi vilivyo kwenye doria Selous kushiriki uokoaji
“Mashuhuda wa ajali ya helikopta Selous walikuwa Kitalu R2 wanasema ilianguka baada ya majira ya saa 12 jioni na kulipuka, serikali kupitia wizara ya maliasili na utalii inachukua hatua zote kuwafikia wahanga na majeruhi wa ajali ya helikopta Selous usiku huu
“Nimeagiza section 2 zenye askari 16 kutoka Matambwe na Msolwa (Selous) kwenda eneo la tukio, RPC Morogoro na mkuu kanda ya Msolwa (Selous) wanashirikiana, hatujui kitakachokuwa kimewapata wasafiri ndani ya helikopta iliyoanguka akiwepo Mh, Filikunjombe, tuungane kuwaombea kwa Mungu”

Zaidi pia na Msemaji wa Kampeni za CCM, January Makamba majira ya ya saa sita usiku kupitia ukurasa wake aliandika:

    “Tumesikia habari za chopa kuanguka huko Selous. Mungu aepushe kusiwe na majeruhi. Chopa zote zinazotumiwa na CCM kwenye kampeni ziko salama”

Baadae aliandika: ”Kwakuwa ilisemekana kuwa chopa ya kampeni ya CCM imeanguka, tulifuatilia/kubaini/kuripoti kuwa tulizokodi kama Chama hakuna iliyoanguka.”  Hiyo ndio ilikua tweet ya mwisho kuandikwa na January Makamba usiku lakini badae aliretweet kilichoandikwa na Waziri Nyalandu.

Hata hivyo Kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo  Zitto Kabwe.

 

 Aliandika: “Naomba utulivu.(1) ajali ya helkopta imethibitishwa (2) kuwaka hakujathibitishwa (3) ndugu yangu Deo alikuwamo (4) hakuna uthibitisho wa madhara, naomba utulivu mpaka tupate taarifa rasmi zilizothibitishwa na mamlaka husika, naomba sana hilo ili kuepuka sintofahamu”

Meya wa Ilala, Jerry Silaa asubui aliandika Instagram kuwa; “Baba yangu Capt. William Silaa na Mhe. Deo Filikunjombe na abiria wengine walipata matatizo ya engine ya Helicopter  5Y – DKK jana jioni wakitokea Dar kuelekea Ludewa. Taarifa za mwisho ilionekana imeanguka kwenye msitu wa Selous. Hakuna mawasiliano ya simu. Usiku kucha vyombo vyote vya serikali vimeenda na jitihada za kufika eneo la tukio na jitihada kubwa zaidi zinaendelea asubuhi hii. Nawaomba wote kuwa watulivu kwani jambo hili linahitaji umakini wa hali ya juu na ushirikiano wa taasisi nyingi za wizara tofauti.Tuwaombee Mungu awanusuru.”

 HABARI ZAIDI:

Mbunge wa jimbo la Ludewa, Deo Filikunjombe na Capt. William Silaa (Baba yake Jerry Slaa), wamethibitika kupoteza maisha kwa ajali hiyo. Deo anakuwa mbunge wa sita kupoteza maisha katika kipindi hiki cha uchaguzi mkuu.


UTHIBITISHO ZAIDI:

 Jerry Silaa




“Kwa masikitiko makubwa nimepokea taarifa rasmi kutoka kwa timu ya uokoaji imefanikiwa  kufika katika eneo la ajali na kukuta abiria wote na rubani wamepoteza maisha.
Nimepoteza Baba na rubani mzuri wa nchi yetu Capt William Silaa, nimepoteza rafiki na kiongozi wangu Mh. Deo Filikunjombe. Nawapa pole wote waliopoteza ndungu zao.
Nawaombea marehemu mapumziko ya Amani.
Nawashukuru wote walioshirikiana na familia kusaidia uokozi.
Namshukuru Mh. Rais Jakaya M Kikwete, Dr. John Pombe Magufuli, IGP Ernest Mangu, Katibu Mkuu MU Dr. Meru, Kampuni ya Everest Aviation, Wabunge, MADC, Maafisa wa TCAA na wote walioshiriki kuwatafuta wahanga wa tukio hili.
Tutajuzana taarifa na mipango mingine.” Jerry Silaa ndiye aliyekuwa mtu wa mwanzoni kabisa kuthibitisha taarifa hizo kupitia ukurasa wake wa Instagram.


Naye mjumbe wa Kamati ya kampeni ya CCM, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Wizara ya Sayansi Teknolojia na Mawasiliano,  January Makamba alitweet taarifa hizo.

January Makamba

 



Nimetoka kupokea taarifa inayothibitisha kwamba chopa aliyokuwa amekodi Ndugu yetu Filikunjombe imeanguka na watu wote wamefariki. 


Waliofariki katika helikopta hiyo yenye namba 5Y-DKK ni pamoja na rubani, Kapteni William Silaa, ambaye ni baba wa mgombea ubunge wa Ukonga kupitia CCM, Jerry Silaa na abiria wengine wawili.
Akithibitisha taarifa hizo kwa vyombo vya habari, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo ya Polisi, Paul Chagonja, alisema rubani, Kapteni Silaa aligundua hitilafu ya ndege hiyo mapema na alitoa taarifa kwa uongozi wa pori la Selous, lakini kabla hajapata msaada mawasiliano yalikatika na helikopta ikaanguka.
“Rubani wa helikopta hiyo alitoa taarifa mapema ya kuomba kutua kwenye uwanja wa ndege uliomo ndani ya pori hilo, lakini ghafla mawasiliano yalikatika. Waokoaji wamefika kwenye eneo la tukio na wamekuta miili ya marehemu ikiwa imeungua vibaya kiasi cha kutotambulika,” alisema Kamishna Chagonja.
Msaidizi wa Filikunjombe, Mathias Luoga, alisema helikopta hiyo iliyokuwa na abiria watatu na rubani ilikuwa ikitokea Dar es Salaam kwenda Njombe, lakini wakiwa angani katika eneo la Kilombero ikapata hitilafu na kuanguka katika Mbuga ya Selous.
 Taarifa za awali Meneja wa Selous, Benson Kibonde, ambaye alisema  helikopta hiyo ilianguka karibu na Mto Ruaha, katika Kitalu cha Uwindaji cha R3.
Alisema taarifa za ajali hiyo walizipata kwa njia ya satellite kutoka kwa mwindaji mmoja ambaye akiwa katika hema lake ndani ya Pori la Selous katika Kitalu cha R2, alisikia kishindo cha helikopta ikianguka na kuona moshi upande wa Kitalu cha R3.
Alisema baada ya ajali hiyo kutokea, mwindaji huyo pia alitoa taarifa kwa Kampuni ya Uwindaji ya Foa Adventure ambayo imempeleka katika pori hilo.
Kwa mujibu wa maelezo hayo, kutokana na eneo hilo kuwa karibu na Mto Ruaha, ilikuwa vigumu kwao kwenda kwa kuwa usiku ulikuwa umekwishaingia.

TAARIFA YA TCAA
Katika hatua nyingine, Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), ilitoa taarifa ya kuthibitisha ajali ya chopa hiyo aina ya AS-35.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, chopa iliyopata ajali ilikuwa na namba ya usajili 5Y-DKK, mali ya Kampuni ya General Aviation Service ya jijini Dar es Salaam.
Taarifa hiyo imefafanua kuwa ndani ya chopa hiyo kulikuwa na abiria watatu pamoja na rubani wake ambao wote wamepoteza maisha.
Abiria hao ni pamoja na rubani, Kapteni William Silaa, Deo Filikunjombe, Kasambala Haule na Ediga Mkwela.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa helikopta hiyo iliondoka katika  Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA) saa 9:57 jioni na ilitarajiwa kufika Njombe saa 12:20 jioni.
TCAA ikinukuu taarifa ya  Kituo Kikuu cha kuongozea ndega cha Uwanja wa JNIA, yaani Area Control Centre (ACC), inaelezwa kuwa kilipokea taarifa za awali za ajali hiyo saa 11:54 kutoka kwa mmoja wa watumishi wa Flight  Link, aliyepigiwa simu na shuhuda wa ajali hiyo aliyekuwa kwenye vitalu vya uwindaji wa kitalii huko Selous.
Katika taarifa hiyo, shuhuda wa ajali hiyo alieleza kwamba chopa hiyo ilionekana ikiwaka moto wakati ikielekea kuanguka.
TCAA imesema kuwa timu ya utafiti na uokoaji wa mamlaka hayo kwa kushirikiana na Kampuni ya Ndege ya Everet ya Dar es Salaam ilikutana kwa haraka na  kujipanga kwa ajili ya zoezi la utafutaji na uokoaji  usiku.
Hata hivyo, TCAA ilisema kuwa chanzo cha ajali hiyo bado hakijafahamika na kwamba wataalamu wa uchunguzi wa ajali za ndege wanaendelea na uchunguzi.

HELIKOPTA ILIWAHI KUTUMIWA NA LOWASSA, MBOWE
Taarifa zilizokusanywa na gazeti hili, zinaeleza kuwa kabla ya ajali hiyo, helikopta hiyo iliwahi kutumiwa na wanasiasa maarufu nchini, akiwemo mgombea urais wa Chadema anayewakilisha Ukawa, Edward Lowassa, alipokuwa akitafuta wadhamini wakati akiwania urais kupitia  CCM Juni, mwaka huu.
Pia inaelezwa kuwa helikopta hiyo iliwahi kutumiwa na Chadema katika operesheni zake, ikiwemo ‘Operation Delete CCM’ na nyinginezo.
Zipo pia taarifa zinazoeleza kuwa iliwahi kutumiwa na mgombea ubunge wa Jimbo la Geita, Joseph Kisheku, maarufu kama Msukuma.

MBOWE AELEZA ALIVYOWAHI KUITUMIA
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema chama hicho na kambi ya Ukawa imepokea kwa masikitiko taarifa za ajali hiyo, huku akieleza zaidi jinsi alivyomfahamu Kapteni Silaa.
“Tumepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za msiba huo. Kwa kuwa taarifa zimetolewa na Jerry Silaa, ambaye ni mtoto wa Kapteni Silaa, basi tunaziamini na tumepokea kwa mshtuko mkubwa,” alisema Mbowe na kuongeza:
“Kapteni Silaa naye ninamfahamu… kuondoka kwake ni pigo kubwa kwa sekta ya usafiri wa anga. Alikuwa rubani mzoefu kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati. Amesharusha ndege nchi za Kenya, Uganda hadi Congo. Amesharuka na ndege kwa zaidi ya saa 7,800,” alisema Mbowe.
Alisema licha ya ajali hiyo, Kapteni Silaa pia alipata ajali akiwa na Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari Julai 7.
“Tumefanya naye kazi sana kwenye operesheni zetu na amekuwa akifanya kazi bila kinyongo chochote. Kama unakumbuka kuna ajali ya helikopta aliyopata Mbunge Nassari, Kapteni Silaa ndiye alikuwa rubani na alifanikiwa kuepusha madhara. Isitoshe yule ni kaka yangu wa nyumbani, tunatoka wote Jimbo la Hai na tunashirikiana kwa mambo mengi,” alisema Mbowe.
Kuhusu Filikunjombe, Mbowe alisema alikuwa ni rafiki mkubwa wa kambi ya upinzani, licha ya kuwa chama tawala.

No comments:

Post a Comment