HELIKOPTA ILIYO ANGUKA NAKUPELEKEA VIFO VYA: Aliyekuwa Mbunge wa jimbo la Ludewa, Mhe. Deo Filikunjombe
(43), Plasdius Ngabuma Haule na Egdi Francis Mkwera aliyetajwa kuwa
Ofisa Tawala wa Wilaya ya Tarime na rubani Kapteni William Silaa.
Chopa iliyo kuwa ikitumiwa na Mbunge wa CCM jimbo la Ludewa Deo Filikunjombe ilianguka usiku tarehe 15/10/2015 na kulipuka kwenye mbuga ya Wanyama ya Selous.
Kwa mujibu wa Waziri wa maliasili na utalii Lazaro Nyalandu
alithibitisha kwamba mmoja wa waliokuwemo ndani ni Mbunge wa Ludewa Deo
Filikunjombe.
|
Mh. Deo Filikunjombe
1972 - 2015 |
|
Waziri Nyalandu |
Kupitia ukurasa wake wa Twitter,Nyalandu aliandika;
“Tumetuma vikosi vya maafisa na maaskari katika eneo la Selous
kulikotokea ajali ya helikopta katika harakati za uokozi, ajali ya
helikopta imetokea katika kitalu R3 ndani ya mbuga ya Selous na
mashuhuda wanasema ilianguka na kulipuka ng’ambo ya mto Ruaha....
Mashuhuda wa ajali ya helikopta iliyotokea Selous walikuwa kitalu
R2 na walishuhudia ikianguka na kulipuka ng’ambo ya mto Ruaha Kitalu
R3, Maafisa na Maaskari wanaelekea eneo la tukio kutokea Msolwa na
Matambwe na tumeagiza vikosi vilivyo kwenye doria Selous kushiriki
uokoaji
“Mashuhuda wa ajali ya helikopta Selous walikuwa Kitalu R2
wanasema ilianguka baada ya majira ya saa 12 jioni na kulipuka, serikali
kupitia wizara ya maliasili na utalii inachukua hatua zote kuwafikia
wahanga na majeruhi wa ajali ya helikopta Selous usiku huu
“Nimeagiza section 2 zenye askari 16 kutoka Matambwe na Msolwa
(Selous) kwenda eneo la tukio, RPC Morogoro na mkuu kanda ya Msolwa
(Selous) wanashirikiana, hatujui kitakachokuwa kimewapata wasafiri ndani
ya helikopta iliyoanguka akiwepo Mh, Filikunjombe, tuungane kuwaombea kwa Mungu”
Zaidi
pia na Msemaji wa Kampeni za CCM, January Makamba majira ya ya saa sita usiku
kupitia ukurasa wake aliandika:
“Tumesikia habari za chopa kuanguka huko Selous. Mungu
aepushe kusiwe na majeruhi. Chopa zote zinazotumiwa na CCM kwenye
kampeni ziko salama”
Baadae aliandika: ”Kwakuwa ilisemekana kuwa chopa ya kampeni ya CCM
imeanguka, tulifuatilia/kubaini/kuripoti kuwa tulizokodi kama Chama
hakuna iliyoanguka.” Hiyo ndio ilikua tweet ya mwisho kuandikwa na
January Makamba usiku lakini badae aliretweet kilichoandikwa na Waziri
Nyalandu.
Hata hivyo Kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo Zitto Kabwe.
Aliandika:
“Naomba utulivu.(1) ajali ya helkopta imethibitishwa (2) kuwaka
hakujathibitishwa (3) ndugu yangu Deo alikuwamo (4) hakuna uthibitisho
wa madhara, naomba utulivu mpaka tupate taarifa rasmi zilizothibitishwa
na mamlaka husika, naomba sana hilo ili kuepuka sintofahamu”
Meya wa Ilala, Jerry Silaa asubui aliandika Instagram kuwa; “Baba
yangu Capt. William Silaa na Mhe. Deo Filikunjombe na abiria wengine walipata
matatizo ya engine ya Helicopter 5Y –
DKK jana jioni wakitokea Dar kuelekea Ludewa. Taarifa za mwisho ilionekana
imeanguka kwenye msitu wa Selous. Hakuna mawasiliano ya simu. Usiku kucha
vyombo vyote vya serikali vimeenda na jitihada za kufika eneo la tukio na
jitihada kubwa zaidi zinaendelea asubuhi hii. Nawaomba wote kuwa watulivu kwani
jambo hili linahitaji umakini wa hali ya juu na ushirikiano wa taasisi nyingi
za wizara tofauti.Tuwaombee Mungu awanusuru.”
HABARI ZAIDI:
Mbunge wa jimbo la Ludewa, Deo Filikunjombe na Capt. William
Silaa (Baba yake Jerry Slaa), wamethibitika kupoteza maisha kwa ajali hiyo. Deo
anakuwa mbunge wa sita kupoteza maisha katika kipindi hiki cha uchaguzi mkuu.
UTHIBITISHO ZAIDI:
Jerry Silaa
“Kwa masikitiko makubwa nimepokea taarifa rasmi kutoka kwa
timu ya uokoaji imefanikiwa kufika
katika eneo la ajali na kukuta abiria wote na rubani wamepoteza maisha.
Nimepoteza Baba na rubani mzuri wa nchi yetu Capt William
Silaa, nimepoteza rafiki na kiongozi wangu Mh. Deo Filikunjombe. Nawapa pole
wote waliopoteza ndungu zao.
Nawaombea marehemu mapumziko ya Amani.
Nawashukuru wote walioshirikiana na familia kusaidia uokozi.
Namshukuru Mh. Rais Jakaya M Kikwete, Dr. John Pombe
Magufuli, IGP Ernest Mangu, Katibu Mkuu MU Dr. Meru, Kampuni ya Everest
Aviation, Wabunge, MADC, Maafisa wa TCAA na wote walioshiriki kuwatafuta
wahanga wa tukio hili.
Tutajuzana taarifa na mipango mingine.” Jerry Silaa ndiye aliyekuwa mtu wa mwanzoni kabisa kuthibitisha taarifa hizo kupitia ukurasa wake wa Instagram.
Naye mjumbe wa Kamati ya kampeni ya CCM, ambaye pia ni Naibu
Waziri wa Wizara ya Sayansi Teknolojia na Mawasiliano, January Makamba alitweet taarifa hizo.
January Makamba
Nimetoka kupokea taarifa inayothibitisha kwamba chopa
aliyokuwa amekodi Ndugu yetu Filikunjombe imeanguka na watu wote wamefariki.
Waliofariki katika helikopta hiyo yenye namba 5Y-DKK ni
pamoja na rubani, Kapteni William Silaa, ambaye ni baba wa mgombea
ubunge wa Ukonga kupitia CCM, Jerry Silaa na abiria wengine wawili.
Akithibitisha taarifa hizo kwa vyombo vya habari, Kamishna wa
Operesheni na Mafunzo ya Polisi, Paul Chagonja, alisema rubani, Kapteni
Silaa aligundua hitilafu ya ndege hiyo mapema na alitoa taarifa kwa
uongozi wa pori la Selous, lakini kabla hajapata msaada mawasiliano
yalikatika na helikopta ikaanguka.
“Rubani wa helikopta hiyo alitoa taarifa mapema ya kuomba kutua
kwenye uwanja wa ndege uliomo ndani ya pori hilo, lakini ghafla
mawasiliano yalikatika. Waokoaji wamefika kwenye eneo la tukio na
wamekuta miili ya marehemu ikiwa imeungua vibaya kiasi cha
kutotambulika,” alisema Kamishna Chagonja.
Msaidizi wa Filikunjombe, Mathias Luoga, alisema helikopta hiyo
iliyokuwa na abiria watatu na rubani ilikuwa ikitokea Dar es Salaam
kwenda Njombe, lakini wakiwa angani katika eneo la Kilombero ikapata
hitilafu na kuanguka katika Mbuga ya Selous.
Taarifa za awali
Meneja wa Selous, Benson Kibonde, ambaye alisema helikopta hiyo
ilianguka karibu na Mto Ruaha, katika Kitalu cha Uwindaji cha R3.
Alisema taarifa za ajali hiyo walizipata kwa njia ya satellite kutoka
kwa mwindaji mmoja ambaye akiwa katika hema lake ndani ya Pori la
Selous katika Kitalu cha R2, alisikia kishindo cha helikopta ikianguka
na kuona moshi upande wa Kitalu cha R3.
Alisema baada ya ajali hiyo kutokea, mwindaji huyo pia alitoa taarifa
kwa Kampuni ya Uwindaji ya Foa Adventure ambayo imempeleka katika pori
hilo.
Kwa mujibu wa maelezo hayo, kutokana na eneo hilo kuwa karibu na Mto
Ruaha, ilikuwa vigumu kwao kwenda kwa kuwa usiku ulikuwa umekwishaingia.
TAARIFA YA TCAA
Katika hatua nyingine, Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA),
ilitoa taarifa ya kuthibitisha ajali ya chopa hiyo aina ya AS-35.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, chopa iliyopata ajali ilikuwa na namba ya
usajili 5Y-DKK, mali ya Kampuni ya General Aviation Service ya jijini
Dar es Salaam.
Taarifa hiyo imefafanua kuwa ndani ya chopa hiyo kulikuwa na abiria watatu pamoja na rubani wake ambao wote wamepoteza maisha.
Abiria hao ni pamoja na rubani, Kapteni William Silaa, Deo Filikunjombe, Kasambala Haule na Ediga Mkwela.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa helikopta hiyo iliondoka katika Uwanja wa
Ndege wa Julius Nyerere (JNIA) saa 9:57 jioni na ilitarajiwa
kufika Njombe saa 12:20 jioni.
TCAA ikinukuu taarifa ya Kituo Kikuu cha kuongozea ndega cha Uwanja
wa JNIA, yaani Area Control Centre (ACC), inaelezwa kuwa kilipokea
taarifa za awali za ajali hiyo saa 11:54 kutoka kwa mmoja wa watumishi
wa Flight Link, aliyepigiwa simu na shuhuda wa ajali hiyo aliyekuwa
kwenye vitalu vya uwindaji wa kitalii huko Selous.
Katika taarifa hiyo, shuhuda wa ajali hiyo alieleza kwamba chopa hiyo ilionekana ikiwaka moto wakati ikielekea kuanguka.
TCAA imesema kuwa timu ya utafiti na uokoaji wa mamlaka hayo kwa
kushirikiana na Kampuni ya Ndege ya Everet ya Dar es Salaam ilikutana
kwa haraka na kujipanga kwa ajili ya zoezi la utafutaji na uokoaji usiku.
Hata hivyo, TCAA ilisema kuwa chanzo cha ajali hiyo bado
hakijafahamika na kwamba wataalamu wa uchunguzi wa ajali za ndege
wanaendelea na uchunguzi.
HELIKOPTA ILIWAHI KUTUMIWA NA LOWASSA, MBOWE
Taarifa zilizokusanywa na gazeti hili, zinaeleza kuwa kabla ya ajali
hiyo, helikopta hiyo iliwahi kutumiwa na wanasiasa maarufu nchini,
akiwemo mgombea urais wa Chadema anayewakilisha Ukawa, Edward Lowassa,
alipokuwa akitafuta wadhamini wakati akiwania urais kupitia CCM Juni,
mwaka huu.
Pia inaelezwa kuwa helikopta hiyo iliwahi kutumiwa na Chadema katika
operesheni zake, ikiwemo ‘Operation Delete CCM’ na nyinginezo.
Zipo pia taarifa zinazoeleza kuwa iliwahi kutumiwa na mgombea ubunge wa Jimbo la Geita, Joseph Kisheku, maarufu kama Msukuma.
MBOWE AELEZA ALIVYOWAHI KUITUMIA
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema chama hicho na kambi ya
Ukawa imepokea kwa masikitiko taarifa za ajali hiyo, huku akieleza
zaidi jinsi alivyomfahamu Kapteni Silaa.
“Tumepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za msiba huo. Kwa kuwa
taarifa zimetolewa na Jerry Silaa, ambaye ni mtoto wa Kapteni Silaa,
basi tunaziamini na tumepokea kwa mshtuko mkubwa,” alisema Mbowe na
kuongeza:
“Kapteni Silaa naye ninamfahamu… kuondoka kwake ni pigo kubwa kwa
sekta ya usafiri wa anga. Alikuwa rubani mzoefu kwa nchi za Afrika
Mashariki na Kati. Amesharusha ndege nchi za Kenya, Uganda hadi Congo.
Amesharuka na ndege kwa zaidi ya saa 7,800,” alisema Mbowe.
Alisema licha ya ajali hiyo, Kapteni Silaa pia alipata ajali akiwa na Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari Julai 7.
“Tumefanya naye kazi sana kwenye operesheni zetu na amekuwa akifanya
kazi bila kinyongo chochote. Kama unakumbuka kuna ajali ya helikopta
aliyopata Mbunge Nassari, Kapteni Silaa ndiye alikuwa rubani na
alifanikiwa kuepusha madhara. Isitoshe yule ni kaka yangu wa nyumbani,
tunatoka wote Jimbo la Hai na tunashirikiana kwa mambo mengi,” alisema
Mbowe.
Kuhusu Filikunjombe, Mbowe alisema alikuwa ni rafiki mkubwa wa kambi ya upinzani, licha ya kuwa chama tawala.