Mwalimu Nyerere alifanya mambo mengi makubwa, kitaifa na kimataifa
Alifikiri mambo ndiyo maana hakuwa na mzaha katika maamuzi yake.
Alipenda amani iwepo kila mahali hata baada ya Tanganyika kupata uhuru, akasema asingejivunia hilo hadi pale Afrika nzima itakapokuwa huru.
Akaamua kuja na wazo la kuziunganisha Tanganyika na Zanzibar ili uwe mfano thabiti wa kile alichokuwa anakipigania.
Alipenda usawa kwa hali na mali, ndiyo maana haikushangaza alipoanzisha Azimio la Arusha mwaka 1967 na kutaifisha uchumi uliokuwa mikononi mwa wachache huku walio wengi wakiwa katika umaskini mkubwa.
NI miaka 15 tangu Baba wa Taifa , Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alipofariki dunia katika Hospitali ya St. Thomas jijini London kwa ugonjwa wa saratani ya damu (leukemia).
Alipigania kwa nguvu zote Muungano wa Tanganyika na Zanzibar (Muungano wa Tanzania) wenye umri wa miaka 50 tangu 1964.
Katika miaka ya mwisho ya uhai wake hili lilionekana dhahiri ambapo alilifanya kwa vitendo, si maneno peke yake. Mwaka uliofuata wakati wa uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi alifikia mahala akasimama kidete, akisaidiana na wanachama wengine wa CCM (pengine waliopata nguvu kuona Nyerere yupo nyuma yao), wakazima jaribio la rais wa Zanzibar wa wakati ule Dk. Salmin Amour Juma aliyetaka kuifanyia marekebisho Katiba ya Serikali ya Mapinduzi ili apate nafasi nyingine ya kugombea urais kwa mara ya tatu ifikapo mwaka 2000.
Wakati wa uchaguzi mkuu wa CCM wa mwaka 1997 Mwalimu alilazimika kwenda mwenyewe Chimwaga, Dodoma ingawa hakuwa amealikwa, na kwenda kuzima majaribio kadhaa yaliyokuwa yameandaliwa na “vijana” wa chama hicho kutaka kumng’oa Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, John Samuel Malecela, na badala yake wakapanga wamchague Waziri Mkuu wa wakati huo, Fredrick Sumaye. Akafanikiwa.
Mambo haya yote yalimuudhi na kumkera sana Mwalimu kwa sababu aliamini, japokuwa hakuwa kwenye wadhifa wowote - si wa chama au serikali - kwamba kama asingesimama kidete ustawi wa Muungano, ambao ulikuwa umeanza kutishiwa tena kama ilivyokuwa miaka ile ya 1980, basi ungetetereka. Sasa CCM imeendelea kusimama kidete yenyewe inajitetea kwamba hoja ya Muungano wa Tanzania inasimama juu ya msingi wa sera ya chama hicho, ambayo inaelezwa kwamba ina ncha mbili; yaani kuulinda na kuudumisha Muungano wenyewe kwa upande mmoja na muundo wa Muungano huo kuwa wa Serikali mbili kwa upande wa pili.
CCM inaushabikia Muungano na kupania kuulinda na kuudumisha kwa sababu kwanza inaamini kuwa Muungano huo ni wa watu wenyewe na pili, uliasisiwa na vyama wazazi wake, yaani TANU na ASP.
Inaunga mkono muundo wa Muungano wa Serikali Mbili kwa sababu kwanza ndio ulioamuliwa na waasisi wa Muungano, Mwalimu Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume.
Japokuwa CCM inajinasibu kwamba muundo wa serikali mbili umeridhiwa na Watanzania wengi. Kama watu watahusishwa, basi itakuwa wakati huu wa kuelekea Kura ya Maoni katika mchakato wa Rasimu ya Katipa inayopendekezwa na Bunge Maalum la Katiba, ambayo pia imeshuhudia CCM ikipigana kuhakikisha inapita, Lakini kama kweli Muungano huu unapaswa kuwa na mtazamo halisi wa utashi wa wananchi wote, kuna mambo mengi ya kufanya ili kufikia hatua hiyo ambayo haiwezi kuwa kero tena; iwe Muungano unakuwepo au unavunjika. Wananchi wa pande zote wanapaswa kutoa maoni yao katika harakati za kuifanyia marekebisho Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ili watoe mapendekezo yao na muundo bora wanaodhani unafaa kama serikali moja, mbili au tatu.
No comments:
Post a Comment